Thursday, January 08, 2009

Maandamano Oslo

yageuka na kuwa

vurugu tupu!




Jioni ya Alhamisi Januari Nane, kulifanyika maandamano aina mbili mjini Oslo. Maandamano ya kwanza yalifanywa na wanaounga mkono taifa la Israel kujilinda na ugaidi unaofanywa na Hamas dhidi ya Israel. Maandamano haya yalifanyika nje ya Bunge la Norway (Stortinget) sehemu inayoitwa Eidsvollplassen. Bi. Siv Jensen kiongozi wa chama cha wahafidhina wenye mkondo wa siasa kali (Fremskrittspartiet/Progressive Party) alioongoza maandamano haya. Baada ya Siv Jensen kuhutubia, ikaanza vurugu baina ya wanaounga mkono Israel dhidi ya Hamas, na wanaopinga utumiaji wa mabavu wa kijeshi uliokithiri unaofanywa na Israel dhidi wa Wapalestina wanaoishi ukanda wa Gaza. Palitokea vurugu kubwa ambayo haijawahi kuonekana Oslo kwa muda mrefu sana. 

Waandamanaji wa pande zote mbili walitupiana maneno makali na wengine kupigana. Pamefanyika uharibifu mkubwa kwenye maduka yaliyo kwenye mtaa mkuu wa Oslo, Karl Johan, na maduka yaliyo mitaa ya karibu na Karl Johan. Ilibidi polisi kutumia mabomu ya moshi na ya machozi, farasi na magari ya medani za kivita kusambaratisha waaandamanaji. Waandamanaji kadhaa wamekamatwa na polisi na kuswekwa lupango.

Tangu majeshi ya Israel kuanza kuushambulia ukanda wa Gaza, kwa ndege za kivita, kumekuwa na maandamano ya makundi yanayoipinga Israel karibu na ubalozi wa Israel ulioko barabara ya Park (Parkveien) mjini Oslo.

Maandamano mengine ya amani ya kutoa rambirambi kwa waliouawa na kupatwa na majeraha pande zote mbili kwenye mgogoro huo, yalifanyika mita kadhaa toka Bunge la Norway, sehemu iiitwayo Youngstorget. Maandamano haya yalifanyika kwa amani na utulivu na yalihudhuriwa na mamia ya wakazi wa Oslo.

Angalia vurugu za maandamano ya Oslo:






No comments: