Thursday, March 12, 2009

Khaa! Siri ya kijana Ibrahim said kumzaba kibao Rais Mtaafu wa awamu ya Pili, ali Hassan Mwinyi imefichuka baada ya timu ya waandishi wetu kuizamia kwa kina ishu hiyo iliyotokea ndani ya Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam juzi (jumanne).. Pekukua pekua ya vijana wetu wa kazi imebaini kuwa, Ibrahim ambaye ‘zimefyatuka kidogo’ alimfanyia kitu mbaya mzee huyo mstaafu, baada ya kuchukizwa na kauli aliyoitoa kiongozi huyo wa zamani kuhusiana na andiko lililomo ndani ya Biblia.

Mwinyi alitajwa kumkera kijana huyo pale aliponukuu andiko lililomo ndani ya Biblia lisemalo “ . . .akupigaye kofi shavu la kulia mgeuzie na la pili,” jambo lililotafsiriwa na ubongo wa Ibrahim kuwa sawa na mzee huyo kutoka ndani ya mstari wa sherehe aliyokuwa akiihutubia.

Mzee ruksa kama anavyojulikana na wengi, alimwakilisha Rais Jakaya Kikwete katika sherehe za kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Mohamad, zilizofanyika Machi 10, mwaka huu.

“Ibrahim hapendezwi na hotuba za viongozi wa kiislamu kuhamasisha umoja wa kidini, amekuwa akipinga sana suala hili,” alisema mzee mmoja kutoka Msikiti wa Masjid Nnur uliopo Mabibo Farasi jijini Dar es Salaam ambao mtuhumiwa wa tukio hilo amekuwa akisali.

Katika hatua nyingine waandishi wetu walifika nyumbani anakoishi kijana huyo eneo la Mabibo na kuzungumza na baadhi ya ndugu na jirani zake na kubaini kuwa, mtuhumiwa huyo wa shambulio ni mwalimu aliyetajwa kuwa ni mwenye akili nyingi lakini nusu ‘zimeruka’.

Aidha, dada wa Ibrahim aliyeogopa kutaja jina kwa hofu ya kusumbuliwa na vyombo vya dola alisema kuwa, kaka yake alimaliza Kidato cha Sita mwaka juzi katika Shule ya Sekondari ya Wavulana iliyoko Tabora.

Alisema, akiwa masomoni ndugu yake huyo, alikuwa na akili nyingi darasani zilizomuwezesha kushika nafasi ya kwanza mara nyingi, lakini aliposhindwa katika mtihani wake wa mwisho ‘netiweki’ yake kichwani ilikuwa haikamati vema na kuwa kama mtu aliyechanganyikiwa.

Kijana huyo ametajwa kufanya vituko vingi vikiwemo vya kumpiga mama yake mzazi, huku habari zikidai kuwa aliwahi kumpeleka mwanamke kikongwe msikitini na kuwaomba mashekhe wamfungishe ndoa.

Pamoja na kuwa na vituko hivyo, dogo huyo aliyeandika historia ya aina yake hapa nchini ni mwalimu wa masomo ya jioni ‘Tuition’ anayofundisha katika kituo chake alichokipa jina la Ngome Kongwe.

Waandishi wetu walifanikiwa kufika kwenye kituo hicho kilichoezekwa kwa makuti na kufanikiwa kupiga picha tofauti tofauti zikiwemo zile zinazoonekana kwenye ukurasa huu.

Kufuatia tukio hilo la kulaaniwa, baadhi ya wananchi wamekuwa na maswali mengi juu ya namna kijana huyo alivyotekeleza kitendo hicho cha kishenzi kwa kiongozi wa nchi anayeheshimika katika jamii.

Miongoni mwa maswali hayo ni kwa nini kijana huyo ambaye anatambulika na baadhi ya waumini kuwa kidogo ‘zimeteguka,’ alipewa nafasi ya kwenda kuketi eneo la mbele bila uangalizi wa karibu.

Mbali na hilo, baadhi ya wananchi walitatizika na namna askari wa usalama wa taifa walivyomwacha mtuhumiwa huyo hadi kwenda kutekeleza kitendo hicho bila kumdhibiti, ambapo wametaka uchunguzi wa kina ufanywe.

“Tukio hilo ni la aibu kwa taifa letu, lakini aibu zaidi kwa watu wa usalama, maana kama mtu anaweza kumpiga kiongozi kibao atashindwaje kumdhuru kwa silaha?” Alihoji Chacha Zefania mwanajeshi mstaafu mkazi wa Boko jijini Dar es Salaam.

Wakati tunakwenda mtamboni habari kutoka duru za usalama wa taifa zilidai kuwa, baadhi ya maofisa wake waliokuwepo siku ya tukio hilo walikamatwa na kwamba wanahojiwa kwa uzembe.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alieleza katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa, jeshi lake linaendelea kumshikilia Ibrahim kwa uchunguzi zaidi.

Aliongeza kuwa, hatua za awali zilizochukuliwa na jeshi lake ni kumpeleka hospitalini kumpima akili na kuahidi kuwa matokeo zaidi ya uchunguzi yatatolewa baada ya kukamilika.

Tukio la Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi kuzabwa kibao hadharani linafuatia lile lililowahi kumkuta mwaka jana Rais Mstaafu wa Marekani, George Bush ambaye alipigwa kwa kiatu na mwandishi wa habari wakati akihutubia katika mkutano nchini Iraki.

Gazeti hili linalaani vikali shambulio lililofanywa na kijana Ibrahim dhidi ya rais mstaafu na kwamba linaziomba idara zinazohusika na usalama wa raia kufanya uchunguzi wa kina na kuwawajibisha wahusika.


No comments: