Ukahaba:
biashara pekee yenye
mtaji wa asili
Na Dennis Luambano, Rai la wiki hii
KAMA dunia ingekuwa na raha peke yake au shida peke yake, pasingekuwapo maana ya kuishi kwa sababu binadamu angekinai maisha pengine hata kabla ya kuyaonja.
Ili binadamu afurahie maisha, anatakiwa aishi katika dunia ambayo ina mambo yote hayo mawili kwa wakati mmoja kwa kuwa tumeumbwa ili tuhangaike kiakili, kwa mali au kwa nafsi.
Kutokana na hali hiyo, ndio maana binadamu anaweweseka kwa hofu katika maisha yake yote, tajiri ana rasilimali nyingi lakini kuna vitu anavikosa mathalani furaha, na masikini amegandwa na madhila lakini wakati mwingine ana furaha nafsini mwake.
Na kwa kuwa kuna utajiri na umasikini, ndio maana masikini anahangaika ili ayakimbie yanayomsibu na tajiri anahangaika kuhodhi na kuongeza rasilimali zake na wakati mwingine ili zisipotee kabisa.
Mbio hizi za watu wawili, zinaifanya dunia kuwa mahali penye raha na karaha kama nilivyosema mwanzo, na zimesababisha kila mtu kutamani kuishi pengine hadi itakapo angamizwa na mashetani wenye roho mbaya.
Hakika tunapaswa kumshukuru Mola katika hili, kwa kuwa dunia imekuwa kama jalala lenye kila aina ya uchafu ama mto wenye maziwa na asali tamu kama zile za nyuki wadogo, kwani hata mimi napenda kuishi kutokana na yote hayo, je, wewe hupendi kuishi?
Pamoja na yote hayo, kuna jambo moja nataka tulipambanue wote, jambo lenyewe ni ukahaba, sasa sijui niseme kwamba ni raha au ni uchafu unaopatikina katika ulimwengu huu tunaoishi.
Nadhani kila mtu anajua maana ya neno ukahaba ingawa kuna tafsiri nyingi zinazosadifiwa na watu wengine.
Kimsingi, maana ya ukahaba ni umalaya, na iwe kwa wanawake au wanaume, wasichana au wavulana, wazee au vijana, na ulianza zamani kabla ya Masiha hajazaliwa. Si mnakumbuka hadithi ya Sodoma na Gomora inayopatikana kwenye Biblia hasa katika Kitabu cha Agano la Kale?
Ukahaba ukaendelea hata baada ya kuzaliwa kwake na ushahidi wa hili upo, mfano ni yule kahaba aliyetaka kupigwa mawe na Wayahudi wakati Masiha akieneza neno la uzima na kujitambulisha kwamba yeye ni Mwana wa Mungu.
Umeendelea kizazi hadi kizazi na hatimaye unazidi kushamiri hadi kizazi chetu ambacho kuna baadhi ya watu wanakiita ni kizazi cha nyoka! Namna ulivyofanyika nyakati za nyuma na wakati huu ni tofauti kabisa, lakini cha msingi hapa ni kwamba umalaya upo tangu enzi na enzi.
Nyakati za nyuma ulifanyika kwa usiri mkubwa lakini wakati huu hakuna siri tena, kwani kuna baadhi ya nchi zimehalalisha na kuifanya kuwa ni biashara kamili ambayo wahusika wanalipa kodi serikalini.
Wakati baadhi ya nchi zimehalalisha biashara ya ukahaba, Tanzania na baadhi ya nchi nyingine hazijahalalisha shughuli hiyo inayoendelea kufanyika ingawa inapigwa marufuku.
Serikali haiwezi kuruhusu biashara ya ukahaba ifanyike kwa sababu kuu mbili. Siwajibii, lakini ukweli ndio huo, sababu ya kwanza, kuihalalisha ni kwenda kinyume na mila na tamaduni zetu na ya pili ni kujing’ong’a yenyewe kwa kuwa ipo katika kampeni ya kupunguza na kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Hata hivyo, biashara hiyo iwe inafanyika kihalali ama kwa magendo, ukweli unabaki pale pale kwamba ni biashara ya fedhea, aibu na inayotweza utu wa binadamu.
Pamoja na hayo, ukahaba ndio biashara pekee katika dunia hii ambayo ni ya asili kwa maana haitaji mtaji mdogo wala mkubwa kama zilivyo nyingine na wala haihitaji upembuzi yakinifu.
Lakini inaisha na kutoweka pindi muhusika anapozeeka, kwa kuwa akishafikia katika hatua hiyo soko lake linakimbia, na ukahaba unawahusu wanawake na wanaume, kwa hiyo si wanawake peke yao kama wengi wanavyodhani. Kimsingi ukahaba ni kitendo cha kushiriki tendo la ndoa na mwanamume au mwanamke zaidi ya mmoja.
Kwa hiyo, kuna makahaba wa aina nyingi ambao wanafanya shughuli zao kwa mitindo tofauti, kuna wanaojipanga nyakati za usiku katika baadhi ya mitaa hasa inayopatikana manispaa ya Kinondoni.
Kuna wanaopatikana katika nyumba za starehe hususani kumbi za disko, na wengine katika baa zinazouza vinywaji vikali na laini, wengine katika hoteli za kitalii na wengine katika nyumba wanazoishi ambazo wanazigeuza madanguro.
Wengine wanapatikana mitaani, vyuoni, na kuna makahaba wengine ni wake za watu, kwa maana wako ndani ya ndoa lakini wanafanya shughuli hizo na wakati mwingine hata kwa kuhongwa ndimu na muuza genge.
Lakini chanzo cha yote hayo ni nini, je, ni umasikini, eti jinsia ya kike inafanya hivyo ili kujikimu na hali ngumu ya maisha inayowakabili, au ni tamaa waliyonayo ya kutaka kuishi maisha ya gharama na starehe, au ni laana ya asili tuliyopewa na Mola, binafsi sikubaliani na yote hayo, je, wewe mwenzangu unalionaje suala hili la ukahaba?
machweo@yahoo.com
Simu ya kiganja: 0713536577
No comments:
Post a Comment