
Bunge kuamua mafuta
ya Zanzibar
Serikali imesema uamuzi wa kuondoa suala ya mafuta na gesi kwenye orodha ya mambo ya Muungano, lipo mikononi mwa Bunge la Jamhuri la Muungano na si vinginevyo. Ufafanuzi huo wa serikali umekuja siku moja baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kusema kuwa inataka suala la gesi asilia na mafuta liondolewe kwenye orodha ya mambo ya Muungano, kwa kuwa inaona visiwa hivyo havitafaidika na nishati hiyo kama itagundulika visiwani humo.
Akizungumza na HabariLeo jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Muhammed Seif Khatib alisema kama SMZ inataka hivyo, inabidi walifikishe suala hilo kwenye Serikali ya Muungano ili lipelekwe bungeni, lijadiliwe na kisha uamuzi ufikiwe.
“Wanahaki (SMZ) ya kusema walichosema, lakini utaratibu upo wazi, lazima kwanza suala lifikishwe bungeni na Bunge ndilo lenye uamuzi wa mwisho kama kipengele cha Katiba kibadilishwe,” alisema Khatib, ambaye ni mmoja wa mawaziri waandamizi.
“Mimi siwezi kuzungumzia zaidi hisia zao, lakini wana haki ya kikatiba kuzungumza au kujadili suala lolote, lakini jambo hilo lipo kwenye Katiba kama suala la Muungano hivyo lazima itabidi walilete Serikali ya Muungano muswada upelekwe bungeni,” aliongeza Waziri huyo ambaye ni Mbunge wa Uzini Unguja.
Ijumaa iliyopita, Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi wa SMZ, Mansoor Yusuf Himid, aliliambia Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kuwa serikali inapinga ushauri wa Mshauri Mwelekezi aliyetaka suala la gesi na mafuta libaki kuwa jambo la Muungano. Mshauri huyo kutoka Uingereza, Aupec Limited alipewa kazi na serikali kutafuta namna bora ya mgawanyo wa rasilimali ya mafuta na gesi asilia na aliwasilisha ripoti hiyo akitaka jambo hilo libaki kuwa la Muungano, lakini kiundwe chombo kipya kitakachosimamia uchimbaji wa nishati.
Hata hivyo, Himid alisema SMZ haitafuata ushauri huo kwa kuwa inaamini Zanzibar haitanufaika na rasilimali hizo ambazo huenda zikagundulika visiwani humo siku za karibuni. “Katika hili, tumegundua Zanzibar itakosa mapato yake makubwa kwa kampuni za kuchimba ambazo zitasajiliwa Tanzania Bara…hili litainyima mapato mengi Zanzibar,” alisema Himid.
Himid alisema pia kuwa Zanzibar haikubaliani na baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na Mshauri Mwelekezi huyo, kutokana na kuwapo na upungufu kama vile kutofautiana kwa sheria za umiliki wa ardhi kati ya Bara na Zanzibar. Alidai ingawa Katiba ya Muungano inatambua gesi na mafuta kuwa mambo ya Muungano, lakini Tanzania Bara kuna maliasili nyingi kama vile almasi, tanzanite, mafuta na gesi ambazo Zanzibar imekuwa haifaidiki nazo.
“Kama itakuwa suala la mafuta na gesi libaki kama jambo la Muungano, basi suala la marekebisho ya katiba linahitajika kwa sababu Zanzibar hainufaiki na nishati hizo,” aliongeza Himid. Kutafutwa kwa Mshauri Mwelekezi kulikuja baada ya kuwapo kwa mijadala ya namna ya kugawana mapato yatokanayo na gesi asilia na mafuta, hatua ambayo ilisababisha kuundwa kwa Tume ya Pamoja kati ya serikali hizo mbili kushughulikia masuala hayo.
No comments:
Post a Comment