Friday, June 12, 2009

Kuvinjari kwenye tovuti

za ngono kwasababisha

jamaa wa usalama, FOST

kuchunguza wizara na ofisi

ya waziri mkuu



Ofisi za serikali na ya Waziri Mkuu wa Norway. Picha na Scanpix.

Shirika la utangazaji la Norway (NRK) limesema kuwa, mfanyakazi mmoja wa wizara ya sheria amekuwa akivinjari kwenye tovuti za ngono akiwa kazini. Hiyo iliamsha ishara kwa idara ya usalama ya jeshi la Norway, FOST (Forsvarets sikkerhetstjeneste) na kuanza kufuatilia nyendo za jamaa huyo kwenye mtandao. Vijana wa kazi wa FOST wakamwonya huyo jamaa. Lakini hiyo imelipua bomu. Hiyo si kazi ya jamaa wa FOST kufuatilia nyendo za kwenye TEKNOHAMA, wizarani na serikalini. Hiyo ni kazi ya Idara ya Usalama wa Taifa (PST, Politiets sikkerhetstjeneste).

Serikali imeshtushwa na hilo na kuona kuwa idara hiyo imekuwa ikiwachunguza, kitu ambacho kinakwenda kinyume na shughuli na majukumu ya FOST. Kitengo makosa ya jinai cha polisi Norway, KRIPOS tayari kimeanza kuangalia kwa mapana na marefu, maovu yaliyofanywa na idara ya usalama ya jeshi la Norway.

Wizara ya sheria na ofisi ya mwanasheria mkuu wamekuwa mabubu kutoa maoni yao juu ya taarifa za NRK.

Hivi majuzi, idara hiyo imeshutumiwa na tayari inachunguzwa kwa kuwafuatilia na kuwachunguza baadhi ya raia wa Norway, na kutoka na maelezo ya vyombo vya habari, hilo ni kosa. Kazi ya FOST ni kuangalia usalama ndani ya jeshi ili kuhakikisha kuwa taarifa na ripoti nyeti haziangukii kwenye mikono ya wasiohusika.

No comments: