Thursday, July 09, 2009

Maiti 13 za ajali ya Yemenia,

zaokotwa ufukweni

Mafia mkoa wa Pwani.




Ndege aina ya Airbus 310 ya Yemenia.


na Kulwa Karedia, Mafia.


MIILI ya watu waliokufa katika ajali ya ndege ya Shirika la Ndege la Yemen, iliyopata ajali na kuzama nchini Comoro na kuonekana katika ufukwe wa bahari ya Hindi, katika ufukwe wa Mafia, mkoani Pwani, imeongezeka na kufikia 13.

Zoezi la uopoaji jana lilikuwa likifanywa na Jeshi la Polisi, Mkoa wa Pwani, na kikosi cha wanamaji cha Dar es Salaam, kwa kutumia ndege moja ya jeshi hilo ya MV. Ngunguri, na helkopta ya MV. Mamba, ambayo ilikuwa ikihamisha maiti wanaoopolewa na kuwapeleka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kuhifadhiwa.

Maiti zaidi ziliokotwa jana ambapo katika Kisiwa cha Kisinge, Kijiji cha Bareni, ziliokotwa maiti tatu, Kijiji cha Jibondo, maiti moja ya mwanamke, wakati katika Kijiji cha Mlali ziliokotwa maiti tatu.

Katika uopoaji huo, maiti nne ziliokotwa eneo la Ziwani, ambapo moja kati yo ilikuwa ya mtoto wa kike wa miaka 10.

Mpaka jana, kulikuwa hakujaokotwa vifaa vya ndege hiyo zaidi ya vile vilivyookotwa juzi, ambavyo ni kiti cha ndege hiyo, na kipande cha bati kilichoandikwa Air Bus 310, iliyotengenezwa mwaka 1997.

Jana, zoezi la uokoaji lilifanyika kwa kusuasua na kwa shida kutokana na kuchafuka kwa bahari na mabaharia kushindwa kutafuta maiti vizuri.

Hata hivyo, taarifa zilizopatikana jana zilieleza kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, iliwasiliana na kikosi cha uokoaji kilichoko katika Kisiwa cha Comoro, ili kifike kwa ajili ya kutoa msaada wa uokoaji.

Miili yote kutokana na kuonekana ni ya raia wa kigeni, inaaminika kuwa ni miongoni mwa abiria 153 waliokuwa ndani ya ndege ya Yemen, iliyopata ajali kwenye Kisiwa cha Comoro kabla ya kuzama baharini.

Wakati huohuo, Magdalena Paul anaripoti kuwa; Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, amesema maiti wa ajali hiyo ya ndege watapokelewa Dar es Salaam na kuhifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili katika chumba maalum.

Alisema Balozi wa Yemen, Abdulah Ally, ameahidi kutoa ushirikiano katika kushughulikia suala hilo ikiwamo utambuzi na uokoaji.

Kutoka Tanzania Daima

No comments: