Tuesday, November 24, 2009

Rais Kikwete ziarani Jamaica


Na Mwandishi Maalum, Kingston, Jamaica


MAPOKEZI makubwa yamemkaribisha Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete wakati alipowasili mjini Kingston kuanza ziara rasmi ya siku nne ya Kiserikali katika Kisiwa cha Jamaica.

Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Norman Manley, Mhe. Rais Kikwete ambaye anafuatana na Mama Salma Kikwete, amepokewa na Gavana Mkuu wa Jamaica, Mhe. Sir Patrick Allen, ON, GCMG, CD; Waziri Mkuu Mhe. Bruce Golding pamoja na Mkuu wa Majeshi.

Mara baada ya kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa ajili ya mapokezi yake kwenye uwanja wa ndege, Mhe. Rais Kikwete amekwenda moja kwa moja kwenye Hoteli ya Jamaica Pegasus, ambako kundi la Watanzania wanaoishi Jamaica limempokea Mhe. Rais kwa nyimbo, vifijo na vigelegele.

Wakati wa ziara yake, Mhe. Rais Kikwete amepangiwa kukutana na Mhe. Sir Patrick Allen, leo , Jumanne, Novemba 24, 2009, ofisini kwa Gavana Mkuu huyo kwenye Jumba la King’s House, kabla ya kushiriki shughuli nyingine nyingi ikiwa ni pamoja na kuhudhuria tamasha rasmi la kitamaduni katika Jumba la Sanaa la Little Theatre.

Kesho, Jumatano, Novemba 25, 2009, Mhe. Rais Kikwete atakutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Golding kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu. Mhe. Golding wa Chama cha Jamaica Labour Party aliingia madarakani mwaka 2007.

Kabla ya kukutana na Waziri Mkuu, Mhe. Rais Kikwete amepangiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi wa Chama cha Upinzani cha Peoples National Party (PNP), Mhe. Portia Simpson Miller, ambaye alipata kuwa Waziri Mkuu wa Jamaica kwa kipindi kifupi.

Kesho hiyo hiyo, Mhe. Rais Kikwete pia atakutana na kufanya mazungumzo na waziri mkuu mwingine wa zamani wa Jamaica, P J. Patterson, ON, OCC, PC, QC ambaye pia anatoka chama cha PNP

Kwenye ziara hiyo, Mhe. Rais Kikwete pia atahutubia Mkutano wa Pamoja wa Bunge la Jamaica (Baraza la Seneti na Baraza la Wawakilishi) na pia atatoa mhadhara maalum kwenye Chuo Kikuu cha Visiwa vya West Indies cha University of West Indies katika kampasi yake kuu ya Mona.

Mhe. Rais Kikwete pia anatarajiwa kupewa Nishani ya Utumishi Uliotukuka ya Order of Excellence ambayo hutolewa kwa heshima maalum na nchi ya Jamaica kwa marais na marais wastaafu.

Mhe. Rais Kikwete vile vile atatembelea Jumba la Makumbusho la mwanamuziki maarufu kuliko wote waliopata kutokea katika Jamaica, marehemu Bob Marley na pia atazindua Kumbukumbu ya Herb McKenly katika shughuli iliyopangwa kufanyika kwenye Uwanja wa Taifa wa Jamaica.

McKenly alikuwa mwanariadha maarufu wa Jamaica ambaye pia alipata kuwa kiongozi wa riadha nchini humo.

Mhe. Rais Kikwete anakuwa Rais wa pili wa Tanzania kufanya ziara rasmi ya kiserikali katika Jamaica. Rais wa kwanza kufanya ziara rasmi ya kiserikali katika Jamaica alikuwa Mwalimu Julius K. Nyerere mwaka 1974.


No comments: