Friday, February 05, 2010

Risiti ya pingu ya Jerry Muro hii hapa



Jeshi la Polisi linazidi kuchemsha!

Kadhia anayoendesha kwa mbwembwe Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, kuhusu mwandishi wa habari za uchunguzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1), Jerry Muro, imezidi kumweka pagumu baada ya risiti ya pingu anayotuhumiwa nayo mwandishi huyo kupatikana.

Hali hiyo inajitokeza baada ya kile alichoapa Kova kwamba hakuna raia anayeweza kumiliki pingu, na kwamba alikuwa na hakika kwamba Muro asingeweza kupeleka risiti hiyo.

Juzi akiendelea na juhudi zake za kuwakamata watuhumiwa na kuwahukumu huku akisema wengine ni “matapeli sugu”, Kova alisema kwamba Muro aliyekamatwa Jumapili iliyopita na kuachiwa kwa dhamana, alikuwa hajawasilisha risiti hiyo.

Uchunguzi wa Nipashe umebaini kwamba Muro alinunua pingu hiyo kihalali kutoka duka la kuuza silaha la Shirika la Mzinga. Shirika hili ni mali ya serikali.

Nipashe imefanikiwa pia kuona risiti aliyopewa Muro kama ushahidi wa ununuzi wa pingu hiyo, ikiwa na namba 34357310. Stakabadhi hiyo ni mali ya serikali pia.

Risiti hiyo iliyotolewa Mei 20, mwaka 2008, inaonyesha kuwa Muro alinunua pingu kwa Sh, 25,000. Muro ambaye amejipatia umaarufu kutokana na kufichua aina tofauti za rushwa, Jumapili iliyopita alikutwa na pingu katika gari alilokuwa akilitumia mara baada ya kukamatwa kwa kudaiwa kutaka fedha kwa njia ya vitisho kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Bagamoyo, Michael Wage.

Wage pamoja na maofisa wa juu wa Halmashauri hiyo mwezi uliopita walifutwa kazi na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwa tuhuma za ufisadi wa kutisha. Bado wanachunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Miongoni mwa rushwa ambazo Muro alizifichua ni zile zilizohusu askari wa usalama barabarani kupokea rushwa.

Kwa mara ya kwanza Muro alifanya kipindi maalum akiwa mfanyakazi wa ITV na kuwanasa askari hao katika barabara kuu ya Morogoro, kati ya Dar es Salaam na Morogoro.

Mara ya pili alifanya kipindi cha usiku wa habari katika barabara kuu mkoani Iringa na kilionyeshwa na TBC1 anakofanya kazi Muro kwa sasa.

Mwaka jana Muro alishinda tuzo ya mwandishi bora wa mwaka na kipindi cha ITV ambacho kilisababisha askari kadhaa walioonekana wakipokea rushwa kufukuzwa, ndicho kilimpandisha ngazi.

Kadhalika kipindi cha TBC1 nacho kimepeleka kilio kwa askari waliomulikwa, na sasa wanachunguzwa kabla ya kufukuzwa kazi kwa kula rushwa.

Kamanda Kova tangu kuibuka kwa kadhia ya Muro ambayo imeacha maswali mengi kutokana na kuendeshwa mno kwa mizengwe, amekuwa akikanyaga sheria ambazo kama kiongozi wa juu wa Jeshi la Polisi anapaswa kuzisimamia.

Kwa mfano Jumatatu Kova alionyesha hadharani bastola anayomiliki Muro kama ambavyo polisi wengi wamekuwa wakionyesha silaha walizokamata kwa watu wanatuhumiwa kwa ujambazi.

Ingawa Kova alikiri kwamba Muro alikuwa anamiliki bastola hiyo kihalali, hakueleza umma ilikuwa na umuhimu gani basi kiutaalam na kiusalama kutoa taarifa za kina za silaha ya raia, ikiwa ni pamoja na uwezo wake wa kubeba risasi na ilikotengenezwa.

Kadhalika, Kova alionekana akijenga hoja kwamba pingu aliyokuwa anamiliki Muro ilikuwa inatiliwa shaka na kukiwa hakuna sheria yoyote Tanzania inayomzuia mtu kumiliki pingu, kifaa hicho si silaha wala hakina ukiritimba wowote wa kukimiliki.

Kova pia anadaiwa kuvunja sheria ya Takukuru ya mwaka 2007 kwa kuwataja watu waliotoa taarifa za rushwa, hivyo kuweka suala zima katika mtihani mkubwa wa kisheria.

Kifungu cha 51(1) (a) cha sheria hiyo, kinazuia kutajwa kwa jina, makazi na anuani ya mtu aliyetoa taarifa kuhusu vitendo vya rushwa au aliyesaidia mamlaka inayohusika kufanikisha kukamatwa kwa mhusika.

Juzi Kova aliwaanika watu wengine wawili aliodai kuwa ni washirika wa Muro katika kutenda uhalifu, na aliwatangaza kwamba ni “mapateli sugu wasiostahili kupewa dhamana”. Kova aligeuka kuwa Polisi na Hakimu wa kuhukumu papo hapo.

Kadhia ya Muro imekuwa ikibadili mwelekeo kila uchao, awali polisi walikuwa wanamtuhumu kwamba alidai rushwa ya Sh. milioni 10, lakini wameshindwa kueleza ni kwa nini hawakuweka mtego ili kumshikisha na pia ni kwa nini suala hilo halikupelekwa Takukuru ambao kisheria ndio mahali hasa pa kushughulikia makosa ya rushwa.

Jana nipashe iliwasiliana na uongozi wa Shirika la Mzinga ambalo linauza pingu hapa nchini, na ulisema upo tayari kumuuzia hata mwandishi kama anazo fedha.

"Wewe kama una hela njoo tutakuuzia pingu, haina shida tatizo lipo katika silaha," alisema Mary Peter, mfanyakazi wa shirika hilo alipoulizwa na Nipashe, jana jioni.

Mary alipoulizwa kama anakumbuka Muro aliwahi kununua pingu kwao, alijibu kwa kifupi kuwa yeye sio msemaji wa shirika hilo.

Kutoka gazeti la Nipashe la Alhamisi 04.02.2010

No comments: