Thursday, March 18, 2010

Oslo, Norway

Mabaunsa watatu watupwa
lupango miezi sita


Mabaunsa watatu waliokuwa kwenye klabu moja ya starehe iitwayo Onkel Donald (Uncle Donald), Universitets gata, wamehukumiwa kifungo cha miezi sita kila mmoja, baada ya kumpiga na kumwumiza jamaa mmoja Mnaijeria kwenye purukushani iliyotokea Machi mwaka jana. Mabaunsa hao wanafanya kazi kwenye kampuni moja ya ulinzi iitwayo; Security Team AS.

Tukio hilo lililotokea mwaka jana, lilinaswa kwenye kamera za ulinzi mitaani (CCTV), linaonyesha jamaa akidundwa na mabaunsa kama sita hivi, baada ya jamaa kukataa kuondoka, walipomwambia amekataliwa kuingia ndani na lazima aondoke.

Upande wa mashtaka unadai kuwa jamaa alikataliwa kuingia ndani kwa sababu za ubaguzi wa rangi, huku upande wa washtakiwa wakidai kuwa jamaa alikuwa amelewa sana alipofika kwenye klabu hiyo. Mahakama imekubaliana na upande wa mashtaka kwenye kesi hii kuwa nguvu zisizo za lazima na ubaguzi wa rangi vilitumika kumkatalia jamaa kuingia kwenye klabu hiyo.

Kumekuwa na matukio mengi ya wageni, haswa Waafrika kukataliwa kuingia kwenye vilabu vya starehe kwa visingizio lukuki.

Baadhi ya sababu wanazotumia kuwakatalia Waafrika ni:

”lazima uwe mwanachama wa klabu”

Au

”mavazi uliyovaa hayaendani na taratibu za mavazi za klabu hii”.

Kitu ambacho kimeonyesha si sababu za kutosha, bali ni sababu tu za kuwakatalia vijana wetu kuingia kwenye vilabu vya starehe.

No comments: