Sunday, March 24, 2013

Rais Xi Jinping wa China kuwasili Tanzania leo ikiwa ziara ya kwanza rasmi nje ya China toka achaguliwe kuwa Rais siku kadhaa zilizopita




Na Eeuteri Mangi na Hussein Makame - Maelezo

Rais wa Jamuhuri ya watu wa China Xi Jinping anataraija kuanza ziara ya kihistoria nchini tangu kuapishwa  kwake kuitumikia  nchi hiyo ambapo katika ziara hiyo atasaini mikataba 17 ya ushirikiano wa  kiuchumi kati ya Serikali za Tanzania na nchi hiyo.

Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa kimataifa Bernard Membe alisema kuwa  ziara hiyo ni ya kwanza barani Afrika  kwa Rais huyo mpya wa China baada ya kuchaguliwa kuliongoza taifa hilo Machi 14 mwaka huu.

Lengo la ziara hiyo ambayo itaanza tarehe 24 hadi 25 Machi mwaka huu ni kukuza uwekezaji  na biashara baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.


Baadhi ya Mikataba hiyo itahusiana na uboreshaji wa sekta ya viwanda, kilimo hasa cha tumbaku ikiwemo kuwatafutia soko wakulima kutoka mikoa ya Tabora na Ruvuma ili waweze kuuza zao hilo katika soko la China.


Waziri Membe alisema kuwa; “Mikataba mingine ni ya kulipatia Shirika la Utangazaji Tanzania zana za kufanyia kazi na kuandaa mazingira ya ujenzi wa bandari ya Bagamoyo itakayounganishwa na reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), reli ya kati na barabara”.


Rais Xi Jinping pia atazindua na kukabidhi rasmi kituo cha Mikutano cha  Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere  chenye ghorofa tatu na kumbi nne za mikutano  zenye uwezo  kupokea washiriki zaidi ya 1800 kilichogharimu dola za kimarekani milioni 29.7 zilizotolewa na Serikali ya China kwa lengo la kumuenzi Mwalimu Nyerere.


Waziri huyo alisema kuwa baada ya kufika nchini Rais Xi Jinping atazungumza na mwenyeji wake Rais Dk. Jakaya Kikwete pamoja na Viongozi Waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na baadaye atahudhuria dhifa ya kitaifa Ikulu Jijini Dar es salaam.


Siku ya pili ya ziara yake Rais Jinping  atazungumza rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk Ali Mohamed Shein pamoja na ujumbe wa viongozi waandamizi kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.


Waziri Membe aliongeza kuwa Rais Jinping atatoa hotuba maalumu kwa Tanzania, Afrika na Dunia kwa ujumla na kuzungumzia sera ya Serikali mpya ya China kwa bara la Afrika ambayo itahudhuriwa na watu kutoka kada mbalimbali ikiwemo Viongozi na Maafisa Waandamizi wa Serikali, Wahadhiri wa Vyuo Vikuu,Wabunge, Viongozi wa Dini na Asasi za Kiraia na Wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali.


“Hotuba hiyo ya Rais wa China ataitoa kwa lugha ya Kichina na kutafsiriwa  kwa lugha ya Kiingereza na Kiswahili ili iweze kuifika dunia nzima, hivyo tunaviomba vyombo vya habari nchini vichukue fursa hiyo kuwa vya kwanza kuutangazia Ulimwengu” alisema Waziri Membe.

Ziara hiyo ya Rais wa Jamhuri ya Watu wa China  ni muendelezo wa uhusiano mzuri kati ya nchi hiyo na Tanzania ulioasisiwa na viongozi  wa mataifa hayo mawili, yaani Mao Zedong wa China na  Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania.


Rais Jinping ataondoka nchini Machi 25 saa 10:40 jioni kuelekea nchini Afrika Kusini kuhudhuria mkutano wa tano wa Wakuu wa Nchi zinazokuwa kwa kasi kiuchumi ambazo ni Brazil, Urusi, India, China na Afrika ya Kusini (BRICS).


No comments: